
Shirika la Human Rights Watch (HRW) linatoa mwito wa dharura kwa ajili ya kulinda raia wa Uvira, jimbo la Sud-Kivu, ambako hali ya usalama inayozorota inatishia maisha ya maelfu ya watu. HRW linahimiza Monusco, mamlaka za Kongo na washirika wa kimataifa kuchukua hatua za haraka na za pamoja.
HRW limeomba kwa msisitizo kwamba Mission ya Umoja wa Mataifa katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo (Monusco) ipeleke bila kuchelewa wataalamu wa haki za binadamu na wa ulinzi wa raia mjini Uvira, Sud-Kivu.
Kwa mujibu wa shirika hilo, hali ya usalama katika mji huo inahitaji majibu ya haraka na ya pamoja ili kuepusha kuongezeka kwa ukatili dhidi ya wakazi wa eneo hilo.
HRW linapendekeza ushirikiano wa karibu kati ya Monusco na mamlaka za Kongo ili kutathmini hatari na kuchunguza vitengo vya jeshi vilivyoko mashinani.
Shirika hilo pia linatoa mwito kwa Umoja wa Ulaya, Umoja wa Afrika na Marekani kuongeza msaada wa kibinadamu na kutumia ushawishi wao wa kidiplomasia kushinikiza serikali za Burundi, Kongo na Rwanda kuweka ulinzi wa raia mbele ya maslahi mengine.
HRW linasisitiza juu ya ulazima wa kuhakikisha mashirika ya misaada ya kibinadamu yanafikishwa bila vizuizi, na kulinda usalama wa watu wanaolazimika kukimbia mapigano.
Aidha, shirika hilo linapendekeza kwamba Marekani, Uingereza, Umoja wa Ulaya na Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa wachukue mara moja vikwazo vipya, mahsusi, dhidi ya viongozi wa Kongo na Rwanda wanaohusika na ukiukaji wa sheria za kimataifa. “Jaribio la M23 la kuonesha udhibiti wake wa Uvira kama njia pekee ya kulinda usalama wa jamii ya Banyamulenge linaonekana kuwa limewaweka raia katika hatari kubwa zaidi ya ukatili na unyanyasaji,” amesema Thomas de Montjoye, mtafiti mkuu wa eneo la Maziwa Makuu katika HRW.
Kwa kuzingatia hali hii, HRW linahimiza mamlaka za Kongo kupeleka vikosi vya usalama vilivyofundishwa kwa umakini na kuchaguliwa kwa nidhamu, vikosi vinavyoweza kulinda kwa ufanisi raia.
Shirika hilo linataka pia kuondolewa silaha na kuvunjwa kwa makundi ya wanamgambo wa kihalifu, pamoja na kufikishwa mahakamani kwa wale wote waliotenda uhalifu dhidi ya raia, ili kurejesha imani na usalama katika eneo hilo.
Emmanuel Kasereka bin Vikingi