
Kiongozi wa upinzani nchini Uganda, Bobi Wine, amethibitisha kuwa ameondoka nchini baada ya uchaguzi wa Januari uliozua utata. Anasema anaogopa kwa maisha yake kutokana na vitisho vya utawala wa Rais Yoweri Museveni, ambaye amekuwa madarakani kwa karibu miaka arobaini.
Kiongozi wa upinzani wa Uganda, Bobi Wine, amethibitisha kwamba aliondoka nchini baada ya uchaguzi wenye utata wa Januari, akisema aliogopa kuuawa.
Akizungumza katika kipindi cha wenzetu wa Newshour kutoka eneo lisilojulikana, baada ya miezi miwili akiwa mafichoni, alisema: “Ilikuwa dhahiri kwamba utawala ulitaka kuniondoa.”
Mwanamuziki wa zamani wa muziki wa pop aliyegeuka mwanasiasa alikuwa tayari ametangaza kukimbia kupitia video aliyochapisha kwenye mtandao wa X. Katika video hiyo, alirudia madai yake kwamba uchaguzi uliibiwa ili kumpa ushindi Rais Yoweri Museveni, aliye madarakani tangu mwaka 1986.
Museveni, mwenye umri wa miaka 81, alitangazwa mshindi kwa kupata asilimia 72 ya kura na aliwashutumu wapinzani kwa kujaribu kupindua matokeo kwa vurugu.
Wine, mwenye miaka 44 na jina halisi Robert Kyagulanyi Ssentamu, aliambia BBC kwamba wakati wa maficho, wafuasi wake walimsaidia: “Walinipa chakula, nguo na kila kitu kingine.”
Alidai Museveni amejitahidi mara kadhaa kumuua na kwamba mwana wa rais huyo, Jenerali Muhoozi Kainerugaba, ametoa vitisho waziwazi. Kainerugaba, ambaye ni mkuu wa jeshi la Uganda, aliwahi kusema kuwa Wine “anatafutwa akiwa hai au amekufa,” bila kumtuhumu kwa kosa lolote, na hata kutishia kumfanyia ukatili wa kumhasi. Baadaye ujumbe huo ulifutwa kutoka akaunti yake ya X.
Baadhi ya maafisa wa serikali walikanusha kuwa vyombo vya usalama vinamtafuta. BBC imeomba polisi kutoa maoni yao kuhusu suala hilo.
Wine aliongeza: “Hata kama niko nje ya Uganda, bado sipo salama kwa sababu najua utawala huu unaweza kuwafuatilia maadui wake wa kisiasa popote walipo.” Alikataa kueleza jinsi alivyotoka nchini ili kulinda wale waliomsaidia.
Alisema familia yake iliondoka “muda mrefu kabla yake,” lakini alionyesha wasiwasi kwa wanachama wa chama chake cha National Unity Platform waliobaki Uganda, akiwemo naibu wake Lina Zedriga, ambaye amemteua kuwa kiongozi wa muda.
“Atasimamia mambo akiwa Uganda, nami nitaendelea kutoa mwongozo kutoka popote nitakapokuwa,” alieleza.
Wine alionyesha nia ya kurejea Uganda, akisisitiza kuwa kuondoka kwake ni kwa muda tu.
Video yake iliyochapishwa Jumamosi kwenye X ilikuwa mara ya kwanza kuonekana hadharani baada ya wiki kadhaa. Katika video hiyo aliomba vikwazo maalum vya kimataifa dhidi ya Museveni.
Alidai kuwa mamlaka zimekuwa zikivamia mara kwa mara nyumba za wafuasi wake, ikiwemo tukio la Alhamisi, na pia zimeweka vizuizi vya barabarani kote nchini. Alisema nyumba yake mjini Kampala bado imezingirwa na wanajeshi tangu siku ya uchaguzi.
Alikanusha kuvunja sheria, akisema: “Kugombea urais si kosa la jinai.”
Baada ya maandamano kupinga matokeo ya uchaguzi, Kainerugaba — anayechukuliwa kama mrithi wa kisiasa wa baba yake — alidai kuwa magaidi 30 kutoka chama cha Wine waliuawa.
Emmanuel kasereka Bin Vikingi