RADIO BEROYA FM

samedi, septembre 5News That Matters
Shadow

Mshikamano wa kitaifa: Tshisekedi aiomba Goma isitegemee tena msaada wa nje pekee

Rais Félix Tshisekedi amezindua Alhamisi mjini Kinshasa Kampeni ya Kudumu ya Mshikamano wa Kitaifa, yenye lengo la kuwasaidia Wakongo milioni 15 walio katika mazingira magumu, wengi wao wakiwa mashariki mwa nchi.

Ni ujumbe unaogusa kwa kina wakazi wa Goma. Kutoka Kinshasa, Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Félix Tshisekedi, amezindua rasmi Kampeni ya Mshikamano wa Kitaifa yenye hadhi ya kudumu.

Lengo la kampeni hiyo ni kukabiliana na janga la kibinadamu lisilo na kifani. Zaidi ya Wakongo milioni 15 wanaishi katika mazingira magumu sana, wakiwa wamekosa mahitaji muhimu yanayowawezesha kuishi maisha yenye heshima. Mkoa wa Kivu Kaskazini ndio unaobeba mzigo mkubwa zaidi wa hali hiyo, ukiwa na takribani watu milioni 2.7 waliokimbia makazi yao katika maeneo yanayozunguka Goma na Masisi.

Kutokana na kupungua kwa ufadhili wa kimataifa, Mkuu wa Nchi anataka kubadilisha mfumo wa kukabiliana na hali hiyo. “Ulinzi wa Wakongo hauwezi kutegemea kikamilifu upatikanaji wa msaada wa nje, ambao kwa asili yake hubadilika-badilika,” alisema. Anatoa wito wa kujenga mfumo “ulio na uwezo mkubwa zaidi wa kujitegemea, endelevu zaidi na wenye uwezo wa kustahimili misukosuko,” unaozingatia “maadili ya Kiafrika ya kusaidiana.”

Kwa mujibu wa Rais Tshisekedi, hatua hiyo ni sehemu ya juhudi za kuimarisha mamlaka na uwezo wa kujitegemea wa taifa, lakini si kujiondoa kwa Serikali katika majukumu yake. “Kampeni hii haichukui nafasi ya majukumu ya kikatiba na kijamii ya Serikali,” alisisitiza.

Katika sehemu iliyogusa hisia za wengi, Tshisekedi alitoa heshima kwa wafanyakazi sita wa mashirika ya kibinadamu waliouawa nchini DRC tangu Januari mwaka huu. “Katika Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, wahudumu wa kibinadamu si walengwa. Hawatakuwa walengwa kamwe,” alisisitiza kwa nguvu.

Umoja wa kitaifa kama ngao dhidi ya mgawanyiko

Zaidi ya suala la michango, Rais anataka kampeni hiyo iwe kiungo cha kuimarisha mshikamano wa kitaifa na kinga dhidi ya mgawanyiko. “Mateso ya raia wenzetu hayajui wala mkoa, kabila, lugha wala dini,” alikumbusha.

“Mkongomani anapokumbwa na dhiki Mashariki, Magharibi, Kaskazini, Kusini au Katikati ya nchi, ni Taifa zima linaloguswa. Tukiwa tumegawanyika, tunajidhoofisha; lakini tukiwa wamoja, tunakuwa nguvu ambayo hakuna jaribu linaloweza kuishinda.”

Rais Tshisekedi pia alitoa wito wa moja kwa moja kwa makampuni ya uchimbaji madini, benki na mawasiliano, pamoja na vijana na Wakongo wanaoishi katika diaspora, kushiriki katika juhudi hizo. “Hakuna mchango ulio mdogo unapofanywa kwa unyofu na upendo.”

Kaulimbiu ya kampeni hiyo ni: « Mchango wako una thamani katika kutoa Tabasamu, Faraja na Matumaini. »

La Reine Aminata Kitambala

Laisser un commentaire

Votre adresse e-mail ne sera pas publiée. Les champs obligatoires sont indiqués avec *