
Burkina Faso, Mali na Niger, wakiwa wameunganishwa chini ya Umoja wa Mataifa ya Sahel (AES), wametangaza operesheni ya kijeshi ya pamoja dhidi ya makundi ya kigaidi. Hatua hii ni ishara ya ujasiri wa kisiasa na kiusalama, miezi michache tu baada ya kuvunja uhusiano wao na CEDEAO pamoja na washirika wao wa zamani wa Magharibi.
Rais wa mpito wa Burkina Faso, Ibrahim Traoré, ametangaza kuwa nchi yake na washirika wake wa Sahel watazindua katika siku chache zijazo operesheni kubwa ya kijeshi dhidi ya makundi ya kigaidi.
Tangazo hili limekuja baada ya mkutano wa kilele wa AES uliofanyika Jumanne, mkutano ulioweka hatua mpya katika mshikamano wa kiusalama kati ya mataifa haya matatu.
Wiki chache kabla ya mkutano huo, Umoja ulikuwa umethibitisha kuundwa kwa jeshi la pamoja lenye askari 5,000, lililokusudiwa kupambana na mashirika yanayohusiana na Al-Qaïda na Dola ya Kiislamu.
Ibrahim Traoré, ambaye sasa amechukua urais wa mzunguko wa AES, hakufafanua kwa undani taratibu za operesheni hiyo, lakini alisisitiza dhamira ya mataifa matatu kushirikiana kwa karibu katika juhudi za kijeshi.
Burkina Faso, Mali na Niger tayari wameidhinisha kujiondoa katika CEDEAO, wakitangaza azma yao ya kujenga mfumo huru wa kikanda.
Zaidi ya sura ya kijeshi, AES inalenga pia kuimarisha uhusiano wa kiuchumi na kimkakati, kwa kuendeleza ushirikiano unaovuka mipaka ya mapambano dhidi ya ugaidi pekee.
Miji mikuu ya mataifa haya matatu pia imevunja uhusiano na washirika wao wa jadi, Ufaransa na Marekani, na sasa imegeukia Urusi, inayotazamwa kama mshirika mkuu katika safari yao ya kutafuta uhuru na uthabiti.
Emmanuel Kasereka bin Vikingi