
Tangazo la ajira linasambazwa kwa kasi kupitia mitandao ya kijamii na programu za mawasiliano, likidai kuwa Wizara ya Utumishi wa Umma ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo (DRC) imefungua mfumo wa kuajiri watumishi katika mikoa mbalimbali ya nchi.
Hata hivyo, tangazo hilo ni utapeli wa mtandaoni unaolenga kuwaibia watafuta kazi taarifa zao binafsi au fedha kwa kutumia matangazo ya ajira ya uongo.
Dalili zinazoonyesha kuwa ni utapeli
Kiungo kisicho rasmi: Anwani ya tovuti inayosambazwa (shrlnk.site) ni kifupisho cha kiungo kisicho rasmi na haihusiani kwa namna yoyote na tovuti rasmi za Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo.
Makosa ya lugha: Picha inayotumika kutangaza ajira hiyo ina maandishi yasiyo sahihi, ikiwemo kauli ya Kireno « CANDIDATE-SE JÁ », inayomaanisha « Omba sasa. » Hili linaonyesha kuwa tangazo hilo limetengenezwa kwa haraka na wahalifu wa mtandaoni au hata kwa kutumia akili mnemba (AI).
Matumizi mabaya ya nembo rasmi: Matapeli hao wametumia kinyume cha sheria nembo rasmi za Serikali na za Wizara ya Utumishi wa Umma ili kulifanya tangazo hilo lionekane kuwa halali.
Kutokana na jaribio hilo la udanganyifu wa kidijitali, Wizara ya Utumishi wa Umma haikukaa kimya. Kupitia taarifa iliyochapishwa kwenye kurasa zake rasmi, imekanusha tangazo hilo, imelielezea kuwa ni udanganyifu unaofanywa na watu wenye nia ovu na kutoa tahadhari kwa wananchi dhidi ya mtandao huo wa kitapeli.
Unapaswa kufanya nini?
– Usibofye viungo visivyothibitishwa vinavyotumwa kupitia WhatsApp, Facebook au mitandao mingine ya kijamii.
– Usitoe taarifa zako binafsi kama kitambulisho, taarifa za benki au namba ya simu kupitia majukwaa yasiyo rasmi.
– Hakikisha unathibitisha taarifa zote zinazohusu ajira kupitia njia rasmi za mawasiliano za Wizara ya Utumishi wa Umma na Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo pekee.
Nzangura Kwavingiston