
FC Barcelona imeibuka mshindi dhidi ya mpinzani wake wa jadi, Real Madrid (3-2), na kutwaa Kombe la Super Hispania kwa mara ya 16 katika historia yake. Kylian Mbappé, aliyeingia uwanjani mwishoni mwa mchezo, hakufaulu kuzuia kichapo cha timu yake.
Kulikuwa na msisimko, mabao na mvutano. Mwishoni mwa clasico yenye umeme wa hisia, iliyowavutia mashabiki waliokuwepo katika uwanja wa Mfalme Abdallah mjini Djeddah, Saudi Arabia, Barcelona ilinyakua taji lake la pili mfululizo kwa kuishinda Real Madrid (3-2), Jumapili hii.
Wakiwa na ari ya kushambulia, vijana wa Hansi Flick walitumia kiungo chao kuzikandamiza juhudi za Madrid na kujenga nafasi za hatari. Hata hivyo, walikwama kwa muda mrefu mbele ya Thibaut Courtois aliyekuwa ngome isiyopenyeka (dakika ya 27, 40). Hatimaye ukuta huo uliporomoka kupitia Raphinha, shujaa wa nusu fainali, aliyepokea pasi ya kifundi kutoka kwa Fermin Lopez (36’).
Lakini Wacatalunya walishuhudia Madrid ikirejea kwa bao la ustadi binafsi la Vinicius, aliyemzunguka Koundé na kufunga bao lake la kwanza (45+2’) baada ya mechi 16 bila kufunga. Dakika mbili baadaye, Robert Lewandowski aliweka Barcelona mbele tena (45+4’). Lakini muda wa nyongeza ulikuwa wa ajabu: Gonzalo Garcia alisawazisha mara nyingine kupitia kona (45+6’).
Mbappé aingia lakini anakaa kimya
Mchezo uliendelea kwa mapambano makali na makosa mengi. Raphinha aliwaokoa Barcelona kwa shuti lililoguswa na Raùl Asencio na kuingia wavuni (73’).
Ili kusaka sare, Xabi Alonso alicheza karata yake ya mwisho. Mbappé, aliyewasili Ijumaa mjini Djeddah licha ya kuhitajika kupumzika wiki tatu, aliingia dakika ya 76 kuchukua nafasi ya Gonzalo Garcia aliyekuwa amekimbia sana.
Hata hivyo, Mfaransa huyo hakufaulu kubadilisha mwelekeo wa mchezo. Hakujenga nafasi ya kufunga, japokuwa alifanya kurudi kwa nguvu za kiulinzi dhidi ya Lamine Yamal na kupata faulo iliyosababisha kutolewa kwa Frenkie de Jong (90’). Lakini juhudi hizo hazikutosha, na Madrid ikashindwa kusawazisha tena.
Obedy Madirisha