
Iran imethibitisha asubuhi ya Jumapili, tarehe 1 Machi 2026, kifo cha Kiongozi Mkuu wa Mapinduzi ya Kiislamu, Ayatollah Ali Khamenei, aliyekuwa na umri wa miaka 86. Tangu mwaka 1989, alisimama kama mrithi wa Ayatollah Ruhollah Khomeini, akibeba mwendelezo wa mfumo wa kidini na kisiasa ulioasisiwa na Khomeini.
Televisheni ya taifa ilitangaza habari hizo saa 05:00 kwa saa za Tehran (01:30 TU). Mtangazaji alisisitiza kwamba “njia na dhamira ya Kiongozi Mkuu hazitapotea wala kusahaulika”, akiongeza kuwa sauti na ujumbe wake vitaendelezwa kwa nguvu na ari mpya. Picha na kumbukumbu za kihistoria zilionyeshwa hewani, zikifunikwa kwa bendera nyeusi ya maombolezo, ishara ya mwisho wa enzi ya kisiasa iliyodumu kwa miongo mitatu na zaidi.
Serikali imetangaza kipindi cha maombolezo ya kitaifa kwa siku 40, pamoja na mapumziko ya siku 7, ili kutoa heshima kwa kiongozi aliyeondoka. Hata hivyo, mazingira halisi ya kifo chake hayakufafanuliwa. Vyombo vya habari vya serikali havikuzungumzia uvumi wa mashambulizi ya pamoja ya Marekani na Israeli yaliyodaiwa kulenga makazi yake mjini Tehran, katika muktadha wa vita vipya vilivyozuka dhidi ya Iran. Kwa mujibu wa RFI, hali hii inahusishwa na mashambulizi hayo ya kijeshi.
Ali Khamenei alipanda ngazi ya uongozi mwaka 1989, baada ya kifo cha Khomeini. Katika kipindi cha utawala wake wa miaka 36, alijenga mamlaka yake kwa kutegemea taasisi za kidini na kijeshi, huku akidumisha msimamo mkali wa kisiasa. Utawala wake uliunda sera ya upinzani mkali dhidi ya Marekani na Israeli, ukasisitiza nafasi ya makasisi katika siasa za ndani na za nje, na kuongeza mvutano wa wazi na mataifa ya Magharibi.
Kifo chake kimefungua ukurasa wa sintofahamu na hatari ya makabiliano ya moja kwa moja ya kisiasa na kijeshi. Iran sasa iko vitani na Marekani na Israeli, jambo linaloongeza uzito wa pengo lililoachwa na Kiongozi Mkuu, mhimili wa mfumo wa Kiirani.
Kuteuliwa kwa mrithi wake kutakuwa kitovu cha mijadala ya ndani, kati ya haja ya kuendeleza mwendelezo wa kiitikadi na jukumu la kusimamia mvutano wa kijiopolitiki. Viongozi wa kidini watalazimika kufikia makubaliano juu ya sura mpya itakayoweza kudumisha uwiano wa taifa na mfumo wake wa kiroho na kisiasa.
Emmanuel Kasereka Bin Vikingi