
Utafiti wa kiwango cha udaktari unaoendeshwa tangu mwaka 2023 na CT Esdras Shabani Bin Kasongo, mhadhiri katika Chuo Kikuu Huria cha Maziwa Makuu (ULGL-Goma), umeonesha kupungua kwa kasi kwa misitu ya mijini na maeneo yanayozunguka mji wa Goma. Utafiti huu unaofanywa katika mpango wake wa udaktari anaoufanya katika chuo kikuu kimoja nchini Kameruni, ambako anajikita katika taaluma ya usimamizi wa misitu, unachunguza namna misitu ya mjini inavyosimamiwa pamoja na mustakabali wake. Matokeo ya awali ya utafiti huo yalitangazwa kupitia mahojiano aliyofanya na wenzetu wa naturelcd.net.
Matokeo ya utafiti huo yanaonesha hali ya kutia wasiwasi: iwapo hakutakuwa na sera madhubuti za kulinda na kurejesha maeneo yenye misitu, mji wa Goma unaweza kupoteza sehemu kubwa ya eneo lake la misitu ifikapo mwaka 2050. Hali hiyo inaweza kuongeza athari za uharibifu wa mazingira, mabadiliko ya tabianchi, kupungua kwa viumbe hai pamoja na kuathiri moja kwa moja maisha ya wakazi.
Makadirio yaliyofanywa katika utafiti huo yanaonesha kuwa eneo lote lenye misitu linaweza kushuka hadi kufikia asilimia 1,74 ifikapo mwaka 2050. Katika maeneo ya mjini, misitu inaweza kubaki kwa kiwango cha asilimia 0,24, huku maeneo ya pembezoni mwa mji yakibaki na takribani asilimia 0,38 pekee. « Tunaelekea moja kwa moja kwenye hatari kubwa ikiwa hakuna hatua zitakazochukuliwa kubadili hali hii, » anaonya CT Esdras Shabani Bin Kasongo.
Ili kufikia hitimisho hilo, mtafiti alichambua mabadiliko ya maeneo ya misitu katika mji wa Goma kwa kipindi cha miaka 35. Matokeo yanaonesha kuwa mwaka 1990, misitu ilikuwa ikichukua asilimia 41,49 ya maeneo ya mjini, lakini kufikia mwaka 2025 kiwango hicho kilishuka hadi asilimia 7,41 pekee. Katika maeneo ya pembezoni mwa mji, hususan Bujovu, Lac Vert na Mugunga, eneo la misitu lilipungua kutoka asilimia 74,8 hadi asilimia 8,41. « Maeneo ya misitu yanabadilishwa hatua kwa hatua kuwa maeneo ya ujenzi, jambo linalosababisha kupungua kwa kasi kwa miti katika mji wa Goma, » anaeleza mtafiti huyo.
Mbali na takwimu hizo, utafiti unaonesha umuhimu mkubwa wa misitu ya mijini katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi. Misitu hiyo husaidia kufyonza hewa ukaa (kaboni), kudhibiti hali ya hewa ya eneo husika, kulinda viumbe hai, kupunguza mmomonyoko wa udongo na kuboresha ubora wa hewa. Utafiti huo pia unalenga kupendekeza mfumo endelevu wa usimamizi unaoweza kuunganisha maendeleo ya miji na uhifadhi wa rasilimali za misitu.
Kwa CT Esdras Shabani Bin Kasongo, uhifadhi wa misitu ya mijini sasa ni jukumu la dharura la kimazingira. Anaona kuwa mamlaka za umma, watafiti, mashirika ya mazingira, washirika wa maendeleo pamoja na jamii zinapaswa kuunganisha nguvu ili kubadili mwenendo huu na kuimarisha uwezo wa Goma kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.
« Ni wakati wa sisi kusimama na kushiriki wote katika shughuli za upandaji miti ili kuokoa maisha ya wananchi na mustakabali wa mji wa Goma, » anahitimisha CT Esdras Shabani Bin Kasongo.
Emmanuel Kasereka bin Vikingi


