
Siku ya pili ya mashindano ya ndani yaliyoandaliwa na Cercle Sportif d’Oïcha ilitoa mapambano ya kusisimua Jumatatu hii, ambapo FC Kasindi ilinyakua ushindi muhimu dhidi ya Lume Sport, huku AS Sukisa na AS Lubiriha wakitoka sare baada ya pambano lenye ushindani mkali.
Michezo ya hatua ya makundi ilipigwa Jumatatu tarehe 05 Januari 2026. Saa saba mchana (13h), AS Sukisa ya Lume ilikabiliana na AS Lubiriha, kisha saa tisa alasiri (15h) FC Lume Sport ikapimana nguvu na FC Kasindi.
Katika pambano la kwanza, AS Sukisa na AS Lubiriha walitoka sare ya bao 1-1. Ndungo Mutalya aliwapa Sukisa uongozi mnamo dakika ya 37, lakini nyota Araphath akasawazisha kwa bao safi dakika ya 78 ya mchezo.
Katika pambano la pili, FC Kasindi Sport iliibuka kidedea kwa bao moja bila majibu dhidi ya FC Lume Sport. Bao pekee lilifungwa na Oscar Kamabu kipindi cha pili, na likawa la ushindi.
Jumapili tarehe 04 Januari 2026, siku ya ufunguzi wa mashindano, kulikuwa na michezo miwili. Saa saba mchana, FC Feu Rouge ya Bulongo ilipoteza mbele ya FC Chui ya Nzenga kwa mabao 3-1. Ushindi huo ulitokana na mabao mawili ya Patrick Mutalinge na jingine la Kambale Basumbe maarufu kwa jina la Isco. Kikosi cha kocha Toto Manopi kilijidhihirisha kwa maamuzi makini na ufanisi mkubwa.
Bao la kwanza lilipatikana dakika ya 29 kupitia penalti iliyowekwa kimiani na Patrick Mutalinge, ambaye aliongeza bao la pili dakika ya 39. Kambale Basumbe Isco alifunga bao la tatu dakika ya 81 na kuhitimisha ushindi wa mabao 3-1 katika muda wa kawaida wa mchezo.
Katika pambano la pili la siku hiyo, AS Ruwenzori ya Mutwanga ilisalimu amri mbele ya Soins Système ya Bulongo kwa bao 1-0. Bao hilo pekee lilifungwa na Kathembo Mupeleka Jadot dakika ya 57 ya mchezo.
Romulus Nzalumbo