
“Kwa moyo thabiti na mshikamano wa kipekee, mabinti wa Virunga wameandika ukurasa mpya wa fahari ya shule. Hatua ya fainali ya mashindano ya mpira wa miguu ya mjini imekuwa alama ya ushindi na ari ya vijana wanaoinua bendera ya taasisi yao.”
Timu ya wasichana ya Complexe Scolaire Children’s Voice Virunga imefanikiwa kufuzu katika fainali ya mashindano ya mpira wa miguu ya mjini. Hatua hii imepokelewa kwa shangwe na pongezi kutoka kwa uongozi wa shule, ambao umeheshimu ari na kujitolea kwa mabinti hawa mashujaa wa michezo.
Shule ya Children’s Voice Virunga imejipambanua katika ulingo wa michezo ya shule kwa kufuzu kwa timu yake ya wasichana hadi hatua ya fainali. Ni matunda ya juhudi, nidhamu na uvumilivu wa wachezaji hawa chipukizi wakiwachapa wale wa Ep Maua kwa bao moja kwa nunge
Katika safari yao ya mashindano, mabinti hawa wameonyesha kipaji cha hali ya juu, nidhamu thabiti na mshikamano wa kipekee wa kikosi. Mechi baada ya mechi, walitoa ushindi wa kuvutia uliowawezesha kupenya hatua zote na hatimaye kufika kilele cha fainali.
Ndani ya shule, habari hii imepokelewa kwa furaha na hamasa kubwa. Walimu, wanafunzi na uongozi wote wamesifu ari ya wachezaji waliobeba kwa heshima bendera ya taasisi yao.
Mkuu wa shule, Fabrice Masivi, alitoa ujumbe wa pongezi na motisha kwa timu:
« Mmejitolea kikamilifu uwanjani. Hongereni kwa kufuzu kwenu katika fainali ya mashindano ya mpira wa miguu ya mjini. Endeleeni kucheza kwa moyo na kwa ujasiri. »
Katika ujumbe wake uliojaa fahari, aliongeza:
« Hongera! Hongera! Hongera! Mko fainali. Mmeonyesha kipaji, mshikamano na ari ya ushindi. Sasa nendeni mkalete kombe nyumbani. Mnastahili ushindi huu. »
Fainali ya mashindano ya mjini sasa inasubiriwa kwa hamu, kama tukio la kihistoria kwa mabinti hawa wanaotaka kuthibitisha uwezo wao na kuliletea taasisi yao taji la ushindi.
Kufuzu huku kunadhihirisha si tu uhai wa michezo katika Children’s Voice Virunga, bali pia nafasi ya michezo katika malezi na ustawi wa wanafunzi.
Emmanuel kasereka Bin Vikingi