
Kutokana na kuongezeka kwa visa vya ugonjwa wa Ebola huko Butembo, Beni na maeneo ya jirani, Jimbo la Butembo-Beni limeimarisha hatua za kinga katika maeneo ya ibada na mikusanyiko ya waumini.
Katika taarifa ya kichungaji iliyotolewa tarehe 13 Agosti 2026, Askofu wa Jimbo la Butembo-Beni, Mgr Melchisédech Sikuli Paluku, amewataka waumini Wakatoliki pamoja na watu wote wenye nia njema kuongeza juhudi za pamoja katika kukomesha kuenea kwa ugonjwa wa Ebola. Wito huo unatolewa wakati ambapo visa vya ugonjwa huo vinaendelea kuripotiwa katika maeneo ya Butembo, Beni na viunga vyake.
Miongoni mwa hatua zilizopendekezwa ni kuwekwa kwa mabeseni ya kunawia mikono au vituo vya maji katika milango mbalimbali ya kuingilia makanisa, mahekalu, makanisa madogo na maeneo mengine yanayotumika kwa mikutano au huduma za kiliturujia. 
Askofu pia amesisitiza umuhimu wa kunawa mikono kwa sabuni au kutumia dawa ya kuua vijidudu kabla ya kuingia kanisani, ili kuimarisha tahadhari za kiafya miongoni mwa waumini.
Jimbo hilo pia limetangaza kusitishwa, hadi hapo itakapotolewa taarifa nyingine, kwa Misa za mazishi zinazofanyika kanisani huku mwili wa marehemu ukiwa ndani ya kanisa.
Hatua hiyo inalenga kupunguza mawasiliano na mikusanyiko ambayo inaweza kuongeza hatari ya maambukizi ya virusi katika kipindi hiki cha tahadhari dhidi ya Ebola.
Hatua nyingine iliyotangazwa ni kwamba sadaka au michango ya waumini itakusanywa baada ya Komunyo.
Taarifa hiyo pia inaagiza kusitishwa, hadi hapo itakapotolewa taarifa nyingine, kwa mikusanyiko mikubwa katika baadhi ya maeneo ya ibada ya jimbo, hususan MCA na Mont Carmel, pamoja na maeneo mengine ya mikusanyiko yaliyotajwa, kama Thabor na Saba.
Shughuli za kwaya na vikundi vya waimbaji pia zimehusishwa katika hatua hizo.
Jimbo linapendekeza kusitishwa kwa muda kwa shughuli hizo, pamoja na zile za MAC na GRAS na safari zao kutoka parokia moja kwenda nyingine. Lengo ni kupunguza mikusanyiko na mienendo ya watu ambayo inaweza kuchangia kuenea kwa virusi katika jamii.
Wakati akitoa wito wa kutekelezwa kwa ukamilifu kwa hatua hizo za kinga, Mgr Sikuli Paluku ameupongeza pia mashirika ya afya na wahudumu wa afya wanaoshiriki katika mwitikio dhidi ya Ebola, na kuwataka wananchi kuwaunga mkono.
Askofu anasisitiza umuhimu wa mshikamano wa pamoja katika kulinda afya ya watu na kuhifadhi maisha ya binadamu. Taarifa hiyo inahitimishwa kwa sala kupitia maombezi ya Bikira Maria, Salus Infirmorum, ili Mungu awahurumie watu walioathirika na kuwabariki.
Emmanuel Kasereka bin Vikingi
