
Mgomo wa madaktari wa hospitali za umma nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo umeingia katika hatua mpya. Kuanzia Jumanne, tarehe 7 Julai 2026, madaktari wamezindua operesheni « Hospitali Bila Madaktari », hatua ya kishirikisho inayolenga kuongeza shinikizo kwa serikali ili itoe majibu ya wazi na ya vitendo kuhusu madai yao ya kijamii na kitaaluma.
Hatua hiyo kulingana na vyanzo kutoka kwa wenziwetu wa Top Congo fm, imechukuliwa na chama cha wafanyakazi wa madaktari baada ya kubaini kuwa mazungumzo yaliyofanyika kati yao na serikali hayajazaa matokeo ya kuridhisha. Madaktari wanasema ahadi walizotarajia kutekelezwa bado hazijapatiwa ufumbuzi, licha ya duru kadhaa za majadiliano.
Kupitia hatua hii mpya ya mgomo, madaktari wanadai kuboreshwa kwa mazingira yao ya kazi, kutekelezwa kwa ahadi zilizotolewa na serikali pamoja na kupatikana kwa suluhisho la kudumu kwa changamoto zinazoikabili sekta ya afya ya umma. Wamesisitiza kuwa huduma za kawaida hazitarejea mpaka madai yao yatakaposhughulikiwa ipasavyo.
Athari za kuimarishwa kwa mgomo tayari zimeanza kujitokeza katika hospitali nyingi za umma mjini Kinshasa na katika majimbo mbalimbali ya nchi. Huduma za kawaida za matibabu zimepunguzwa kwa kiasi kikubwa, huku wagonjwa wa dharura pekee wakiendelea kupatiwa huduma kwa mujibu wa maelekezo ya vyama vya madaktari.
Viongozi wa vyama vya madaktari wameonya kuwa hata huduma za kiwango cha chini zinaweza kusitishwa ikiwa serikali haitatoa majibu yanayoridhisha. Hali hiyo inaweza kuathiri zaidi upatikanaji wa huduma za afya kwa maelfu ya wananchi wanaotegemea hospitali za umma.
Mgogoro huu unatokea wakati ambapo mfumo wa afya wa umma nchini tayari unakabiliwa na changamoto nyingi, zikiwemo uhaba wa rasilimali, matatizo ya ufadhili na ongezeko la mahitaji ya huduma za matibabu. Endapo mzozo huu utaendelea, kuna hofu kwamba shinikizo kwa sekta ya afya litaongezeka zaidi.
Katika mazingira hayo, macho yote sasa yanaelekezwa kwa serikali, ambayo inatarajiwa kurejesha mazungumzo na wawakilishi wa madaktari ili kupata suluhisho la haraka la mgogoro huu. Vyama vya madaktari vimesisitiza kuwa viko tayari kuendelea na mazungumzo, lakini vimeweka wazi kuwa operesheni « Hospitali Bila Madaktari » itasitishwa tu baada ya serikali kutoa majibu ya kuridhisha kwa madai yao.
Elie Mariboyi