
Serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo imechukua hatua mpya katika mkakati wake wa kuongeza thamani ya rasilimali za madini nchini. Kupitia amri ya pamoja ya mawaziri iliyosainiwa tarehe 29 Juni 2026, mamlaka zimepiga marufuku usafirishaji wa makinikia ya shaba na kobalti kwenda nje ya nchi. Hatua hiyo inalenga kuhimiza uchakataji wa madini ndani ya taifa na kuongeza thamani ya bidhaa za madini kabla ya kuuzwa katika soko la kimataifa. Taarifa hizi zimeripotiwa na wenzetu wa Actualité.cd na kuthibitishwa na Beroyafm.net.
Amri hiyo imesainiwa na Naibu Waziri Mkuu anayehusika na Uchumi wa Taifa, Daniel Mukoko Samba, Waziri wa Madini, Louis Kabamba Watum, pamoja na Waziri wa Biashara ya Nje, Julien Paluku Kahongya. Kupitia mageuzi haya, serikali inalenga kuvutia uwekezaji katika viwanda vya ndani vya kuchakata na kusafisha madini, huku ikipunguza usafirishaji wa bidhaa ambazo hazijaongezewa thamani ya kutosha.
Hata hivyo, amri hiyo imeweka uwezekano wa kutoa msamaha maalumu. Wenye leseni za uchimbaji madini, kampuni za uchakataji pamoja na vituo vya ununuzi wa madini wanaweza kuruhusiwa, kwa uamuzi wa Waziri wa Madini, kuendelea kusafirisha baadhi ya bidhaa za madini ambazo hazijachakatwa kikamilifu kwa kipindi kisichozidi mwaka mmoja. Ruhusa hiyo itatolewa tu pale kutakapokuwepo sababu za kiufundi, kiteknolojia au kiuchumi zinazohusiana na shughuli zao.
Aidha, serikali imeanzisha ushuru wa asilimia 55 ya thamani ghafi ya kibiashara ya bidhaa ndogo za madini zenye umuhimu wa kiuchumi. Hizi ni madini yanayopatikana wakati wa kusafisha madini makuu na yenye thamani ya kiteknolojia na kiuchumi. Thamani yake itahesabiwa kwa kuzingatia kiwango cha madini yaliyopo, uzito wa mzigo unaosafirishwa, bei ya kimataifa ya madini husika pamoja na kiwango hicho cha ushuru.
Amri hiyo pia imeweka mfumo mpya wa uainishaji wa bidhaa za madini zinazouzwa, uliogawanywa katika makundi tisa, ikiwemo madini ya msingi, madini ya thamani, kemikali, aloi, makinikia rahisi, makinikia mchanganyiko, madini adimu, bidhaa nyingine za migodi pamoja na madini ghafi na mabaki ya uchimbaji. Viwango vya uthamini vitategemea aina na kiwango cha madini yaliyomo katika kila bidhaa.
Kwa mujibu wa waraka huo, ni wamiliki wa haki za uchimbaji madini, kampuni za uchakataji za daraja B pamoja na vituo vilivyoidhinishwa vya ununuzi na uuzaji wa madini kutoka uchimbaji wa artisanal pekee watakaoruhusiwa kusafirisha bidhaa za madini nje ya nchi. Kipindi cha mpito cha miezi mitatu kimewekwa kabla ya ushuru mpya kuanza kutekelezwa rasmi. Katika kipindi hicho, waendeshaji wataendelea kutangaza bidhaa hizo bila kulipa ushuru huo.
Kupitia mageuzi haya, serikali ya Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo inaonyesha dhamira yake ya kuifanya sekta ya madini kuwa nguzo ya maendeleo ya viwanda, uundaji wa ajira na kuongeza mapato ya taifa. Amri hiyo imefuta masharti yote yaliyokuwa yanakinzana nayo, hususan yale ya tarehe 4 Agosti 2023 yaliyokuwa yakisimamia sekta hiyo, na ilianza kutumika rasmi tangu siku ya kusainiwa kwake.
Idara ya uhariri