RADIO BEROYA FM

mercredi, février 11News That Matters
Shadow

Cotonou Yapokea Kongamano la Kimataifa: Afrika Mstari wa Mbele kwa Ikolojia Shirikishi

Kuanzia tarehe 20 hadi 22 Januari, Taasis ya Jimbo Kuu Katoliki la Cotonou kwa kushirikiana na Chuo Kikuu Katoliki cha Afrika Magharibi (UCAO) wanaratibu kongamano la kimataifa kuhusu ikolojia shirikishi. Mgeni wa heshima, Kardinali Fridolin Ambongo, Askofu Mkuu wa Kinshasa na Rais wa SCEAM, anamulika umuhimu wa mkutano huu wa kihistoria kwa ajili ya uhai na ustawi wa Uumbaji.

Kongamano hili linaendelea katika mwanga wa mwito wa dunia uliotolewa na waraka wa Papa Francisko Laudato Si’, unaohimiza mabadiliko ya kweli ya kiikolojia. Ni jukwaa la tafakuri juu ya uhusiano wa karibu kati ya mazingira, haki ya kijamii na maisha ya kiroho, ili kuendeleza mtazamo wa ikolojia shirikishi kwa ajili ya kulinda Uumbaji.

Waandaaji wanakusudia kuwaleta pamoja watafiti, wanatheolojia, wanaharakati wa kijamii na viongozi wa kisiasa ili kushirikiana katika dira moja: kulinda sayari kwa ajili ya vizazi vya sasa na vijavyo. Mkutano huu unakusudia kuwa wa kiakademia na wa vitendo, ukijaribu kuunganisha tafakuri na matendo halisi.

Mgeni wa heshima, Kardinali Fridolin Ambongo—mbele ya harakati za kiikolojia barani Afrika—anasisitiza juu ya dharura ya mwamko wa pamoja. Kwake, ikolojia shirikishi haijifungii tu katika kulinda mazingira, bali pia inahusu heshima ya utu wa binadamu, mshikamano na haki ya kijamii.

Anabainisha kuwa Afrika, ingawa imebarikiwa kwa urithi mkubwa wa viumbe hai, ni dhaifu zaidi mbele ya misukosuko ya tabianchi. Hivyo basi, bara hili lina wajibu wa kuchukua nafasi ya uongozi katika kulinda Uumbaji, na kutoa suluhisho endelevu huku likiwa mfano wa kupigiwa katika mapambano dhidi ya mabadiliko ya mazingira.

Kwa Benin na ukanda wa Afrika Magharibi, kongamano hili ni fursa ya kuimarisha sera za umma kuhusu ulinzi wa mazingira. Katika upeo wa dunia nzima, linachangia mjadala wa kiulimwengu juu ya uhai wa sayari, kwa kuingiza sauti za Waafrika katika maamuzi makuu ya kimataifa.

Majadiliano yanatarajiwa kuzaa mapendekezo ya vitendo kwa ajili ya Makanisa, Serikali na jamii za mitaa. Lengo kuu ni kuingiza ikolojia shirikishi katika maisha ya kila siku na kutoa mwelekeo wa kivitendo kwa tafakuri zinazofanyika.

Hatimaye, waandaaji wanatumaini kuwa kongamano hili litakuwa kichocheo cha miradi ya kielimu na kijamii. Vijana, hususan, wanaitwa kuwa wahusika wakuu wa mabadiliko haya ya kiikolojia, katika mtazamo wa mshikamano wa kiulimwengu na uwajibikaji wa pamoja.

Emmanuel Kasereka bin Vikingi

Laisser un commentaire

Votre adresse e-mail ne sera pas publiée. Les champs obligatoires sont indiqués avec *