
Mji wa Cantine, ulioko katika kundi la Baswagha-Madiwe, uliyumbishwa tena usiku wa tarehe 23 kuingia 24 Novemba 2025 baada ya ghala la kakao la Florentine kushambuliwa na watu wenye silaha wasiojulikana.
Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa, washambuliaji walijitokeza majira ya saa nane usiku. Baada ya kushindwa kulazimisha mlango kufunguliwa, waliuvunja kwa risasi. Wafanyakazi wawili, Muhindo Kistamuli Alain (miaka 25) na Kambale Noël, walijeruhiwa. Mbwa wa ulinzi naye alipigwa risasi na kuuawa. Waathirika wanapatiwa matibabu katika kituo cha afya cha Cantine.
Licha ya majibu ya vyombo vya usalama, wahalifu walitoroka kwa pikipiki kuelekea Gîte-Lubena, wakiwa wamebeba kiasi kikubwa cha fedha ambacho hakijabainishwa.
Asasi ya kiraia ya Baswagha-Lubena imelaani shambulio hili, ikilitaja kuwa tishio kubwa kwa usalama wa eneo. Mwenyekiti wake, Kambale Musubao Aliamini, ametoa wito wa kufanyika kwa uchunguzi makini na ameonya juu ya uwezekano wa ushirikiano wa ndani:
“Haiwezekani watu wenye silaha wajue kuwepo kwa fedha ndani ya ghala bila ushirikiano wa ndani,” alihitimisha.
Obady Madirisha