
Kwa kuibuka na ushindi mwembamba wa bao 1–0 dhidi ya Benin katika uwanja wa Rabat, Leopards wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo wameweka msingi thabiti na sasa macho yao yameelekezwa kwenye mtanange wa kuamua hatima dhidi ya Senegal, moja ya vigogo wa michuano hii ya CAN 2025.
Rabat, Jumanne. Safari ya Kongo katika Kombe la Mataifa ya Afrika 2025 imeanza kwa mwanga wa ushindi. Bao la pekee lililofungwa na Théo Bongonda limewapa alama tatu muhimu na kuwatia moyo kuelekea pambano linalofuata.
Tangu dakika za mwanzo, Wacongo walitawala mchezo kwa kasi na ustadi wa kiufundi, wakipiga pasi kwa ujasiri na kuonyesha ubora wao. Hatua hiyo ilizaa matunda mapema.
Dakika ya 16, Bongonda alitikisa nyavu kwa kishindo. Kupitia mpira mrefu wa Arthur Masuaku, mshambuliaji wa Spartak Moscow alitumia kosa la ulinzi wa Benin na kumalizia kwa shuti kali la mguu wa kushoto lisilozuilika.
Bao hilo la mapema liliwapa Leopards ujasiri wa kuendelea kushambulia. Walipata nafasi kadhaa za kuongeza idadi ya mabao, lakini bahati haikuwa upande wao, na hivyo kusalia na mvutano hadi mwisho wa mchezo.
Guépards wa Benin hawakukata tamaa. Katika dakika za mwisho walijaribu kusawazisha, wakakaribia kufanikisha, lakini ngome ya Kongo ilibaki imara na makini.
Ushindi huu, ingawa ni mwembamba, ni ishara ya dhamira na ari ya Wacongo katika mashindano haya. Hata hivyo, makali ya safu ya ushambuliaji yanahitaji kuimarishwa zaidi wanapokabiliana na wapinzani wakali zaidi.
Kwa alama tatu walizokusanya tayari, Leopards wanaingia kwenye mtanange dhidi ya Senegal wakiwa na imani na morali ya juu. Wanajua fika kwamba ili kuwashinda vigogo wa soka la Afrika, watapaswa kuongeza kiwango chao, lakini ushindi huu wa mwanzo ni hazina ya kisaikolojia inayowapa nguvu ya kupambana.
Emmanuel Kasereka bin Vikingi