
Burkina Faso imeadhimisha Alhamisi, tarehe 6 Agosti 2026, hafla ya kumi ya kijeshi ya kumuenzi Rais Thomas Sankara pamoja na wenzake kumi na wawili katika Kumbukumbu ya Thomas Sankara mjini Ouagadougou. Hafla hiyo, ambayo sasa imekuwa sehemu ya kumbukumbu ya kitaifa inayofanyika kila mwaka, imewakutanisha viongozi mbalimbali wa serikali ili kuenzi maadili ya uzalendo, uhuru wa taifa, haki ya kijamii na uadilifu yaliyokuwa yakisimamiwa na Baba wa Mapinduzi ya Kidemokrasia na Kijamii ya Agosti 1983.
Sherehe hiyo ilihudhuriwa na Waziri wa Mawasiliano, Utamaduni, Sanaa na Utalii, Pingdwendé Gilbert Ouédraogo, pamoja na Waziri wa Viwanda, Biashara na Ufundi, Serge Gnaniodem Poda, ambaye alikuwa mwenyekiti wa maadhimisho hayo ya kumi. Viongozi hao walisisitiza dhamira ya kuendeleza kumbukumbu ya Kapteni Thomas Sankara na kurithisha urithi wake kwa vizazi vya sasa na vijavyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Waziri Pingdwendé Gilbert Ouédraogo alisema kuwa maadhimisho hayo si sherehe ya kawaida bali ni fursa ya kila raia wa Burkina Faso kufanya tafakari kuhusu mustakabali wa taifa kwa kuzingatia maadili aliyoyaacha Thomas Sankara. Alikumbusha kuwa kiongozi huyo wa zamani alitoa dira ya kujenga taifa lenye heshima, kujitegemea, uwajibikaji na maendeleo yanayotokana na nguvu za wananchi wenyewe.
Kwa upande wake, Waziri Serge Gnaniodem Poda alieleza kuwa hafla hiyo ni wajibu wa kitaifa wa kuhifadhi historia. Alikumbusha kuwa chini ya uongozi wa Thomas Sankara, Burkina Faso ilitekeleza mageuzi muhimu ya kiuchumi, ikiwemo kuandaliwa kwa Sheria ya kwanza ya Uwekezaji pamoja na kuanzishwa kwa Maonesho ya Kimataifa ya Ufundi ya Ouagadougou (SIAO), ambayo leo ni miongoni mwa maonesho makubwa zaidi ya ufundi barani Afrika.
Katika hafla hiyo pia, serikali ilitoa taarifa kuhusu maendeleo ya mradi wa Kumbukumbu ya Thomas Sankara, ambao unalenga kuwa kitovu cha historia, utamaduni na elimu ya uraia. Mbali na makaburi ya heshima, mradi huo unajumuisha ujenzi wa mnara wenye urefu wa mita 87, sanamu 14 zinazomuenzi Thomas Sankara, wenzake kumi na wawili pamoja na Rais wa heshima wa kumbukumbu hiyo, John Jerry Rawlings. Aidha, kutajengwa maktaba, ukumbi wa watu 3,000, ukumbi wa matumizi mbalimbali, kituo cha biashara, bustani ya mimea, eneo la mafunzo ya kihistoria, sehemu za mapumziko na mfumo wa usafiri wa kamba (telepherique).
Mradi huo unaokadiriwa kugharimu faranga za CFA bilioni 117, ni miongoni mwa miradi mikubwa ya kuhifadhi urithi wa kihistoria na kitamaduni nchini Burkina Faso. Katika muktadha huo, Waziri wa Mawasiliano alitoa wito kwa wafanyabiashara wa Burkina Faso, wananchi wanaoishi ughaibuni pamoja na marafiki wa Burkina Faso kuunga mkono kampeni ya « Tofali Langu kwa Sankara » (Ma brique pour Sankara), inayolenga kukusanya rasilimali za kukamilisha ujenzi wa kumbukumbu hiyo.
Kupitia maadhimisho haya ya kumi ya kijeshi, Burkina Faso imeonyesha tena azma yake ya kuhifadhi kumbukumbu ya Thomas Sankara na kuendeleza maadili aliyoyaishi. Kwa mujibu wa serikali, Kumbukumbu ya Thomas Sankara itakuwa mahali pa kuhifadhi historia, kutoa elimu ya uraia, kuhamasisha tafakari na kukuza utamaduni, huku ikiendeleza urithi wa mmoja wa viongozi walioacha alama kubwa katika historia ya Afrika.
Emmanuel Kasereka bin Vikingi