
Sintofahamu iliyotokea Jumanne, tarehe 28 Julai 2026, katika eneo la Metale, karibu na Cantine-Centre, wilayani Beni (Kivu Kaskazini), haikusababishwa na shambulio la waasi wa ADF, kinyume na uvumi uliosambazwa kwenye mitandao ya kijamii. Vyanzo mbalimbali vya eneo hilo vinaeleza kuwa milio ya risasi ilitokana na mvutano kati ya wanajeshi wa FARDC na wapiganaji wa Wazalendo kuhusu udhibiti wa kizuizi (barrière) kilichowekwa katika eneo hilo.
Kwa mujibu wa taarifa zilizokusanywa, kutokuelewana kulianza baada ya wapiganaji wa Wazalendo kuweka nafasi yao katika kijiji cha Mahihi, kilichopo katika groupement ya Baswagha-Madiwe. Uwekaji wa kizuizi katika eneo hilo ulionekana kutokubalika na wanajeshi wa FARDC, hali iliyosababisha kurushiana risasi na kuzua hofu kubwa miongoni mwa wananchi.
Asasi za kiraia za eneo hilo zimesema kuwa hali ya usalama kwa sasa imerejea kuwa shwari. Zimewataka wananchi kubaki watulivu, kuwa waangalifu na kuepuka kusambaza taarifa zisizo na uthibitisho ambazo zinaweza kuongeza hofu miongoni mwa jamii.
Viongozi wa jamii wamekumbusha kuwa, licha ya tukio hilo, tishio la waasi wa ADF bado linaendelea kuwepo katika sehemu hii ya wilaya ya Beni. Hivyo, wamewahimiza wananchi kuendelea kushirikiana na vyombo vya ulinzi na usalama pamoja na kuwa makini dhidi ya uvumi.
Matu Chub D.