
Miaka minne baada ya matukio ya kusikitisha yaliyotokea Kighali, katika kijiji cha Isale-Vuhovi, chefferie ya Bashu (wilaya ya Beni), wakazi wa eneo hilo waliandaa, Alhamisi tarehe 8 Januari 2026, ibada ya kiekumene kwa ajili ya amani ya kudumu.
Shughuli hii ya kiroho ililenga kusali kwa ajili ya utulivu katika eneo ambalo hapo awali liliathiriwa na mapigano ya kivita, mauaji na dhuluma mbalimbali, hali iliyosababisha wakazi wengi kukimbilia maeneo yaliyohesabiwa kuwa salama zaidi, hususan Butungera.
Mwami wa Bashu, Abdoul Paluku Kalemire wa Tatu, alishiriki katika ibada hiyo kupitia mwandishi wake, Kakule Ndeke Yonge. Katika ujumbe wake, kiongozi huyo wa jadi aliwatia moyo wakazi na kuonesha matumaini yake kwamba amani itarejea kwa kudumu katika chefferie nzima. “Tumeshachoka na hali ya kutokuwa na usalama katika eneo hili. Uhamaji wa mara kwa mara wa watu na misukosuko imeleta hasara kubwa. Tumepoteza wapendwa wetu, hasara ni nzito. Hata hivyo, bado nina imani kwamba amani itakuwa halisi katika eneo hilo nzima,” alisema.
Ibada hiyo, iliyoandaliwa na asasi za kiraia za Vuhovi, ilikusanya umati mkubwa wa watu waliomiminika kwa shauku ya kuunga mkono amani.
Obady Madirisha na Fiston Matsande