
Jamii ya kiraia ya Bulengera, mjini Butembo, yatoa mwito wa hatua za dharura kukomesha uhalifu wa kijambazi. Mwenyekiti wake, John Kameta, asisitiza juu ya udhibiti wa silaha haramu na mshikamano thabiti kati ya wananchi na vyombo vya usalama.
Kwa kuzingatia hali ya usalama inayoendelea kuzorota, John Kameta apendekeza ukaguzi wa kina na wa mara kwa mara wa silaha za moto zinazomilikiwa kinyume cha sheria na zinazozunguka katika mitaa ya jimbo.
Aidha, anahimiza kuimarishwa kwa mikakati ya kiusalama kote katika eneo la Bulengera ili kuzuia maafa mapya yasije yakatokea.
Jamii ya kiraia inapendekeza kufanyika kwa mikutano ya karibu na wakazi katika vitongoji, ili kusikiliza maoni yao na kuimarisha ulinzi wa pamoja.
Inasisitiza pia haja ya kudumisha mshirikiano wa karibu kati ya wananchi na vyombo vya usalama, jambo linalochukuliwa kuwa msingi wa kujenga jimbo lenye usalama na mshikamano wa kijamii.
Ripoti ya mwaka ya usalama, iliyotolewa Jumamosi tarehe 2 Januari 2026, yafichua kuwa matukio makubwa 32 yalirekodiwa mwaka 2025, mbali na uvamizi wa majumbani na wizi wa mali.
Miongoni mwa matukio hayo, yapo mauaji 10 (yakiwemo watuhumiwa 3 wa ujambazi, huku visa 5 vikijikita zaidi katika kitongoji cha Askofu), ajali 8 za kikazi katika Mutiri, ajali 6 za barabarani, visa 2 vya “haki ya wananchi” (justice populaire), watu 2 waliojinyonga, miili 2 iliyokutwa bila uhai, na visa 2 vya kuzama majini.
Takwimu hizi zadhihirisha sura nyingi za hali ya kutokuwa na usalama inayosumbua maisha ya kila siku ya wakazi, na zinahalalisha uharaka wa hatua zinazopendekezwa na jamii ya kiraia.
Emmanuel Kasereka bin Vikingi